Maneno na sura yangu yalionyesha hatia niliyokua nayo juu ya kosa hilo. Nilishuhudia wakijipongeza kwa kuwarahisishia kazi na mimi kutolewa kwenye kitanda hicho na kusubiri siku inayofuata nipelekwe mahakamani.
Nikiwa kwenye chumba nilichowekwa kwa ajili ya kusubiri nipandishwe kizimbani siku inayofuata, nilifuatwa na askari na kutolewa. Nilirudishwa kwenye chumba cha mahojiano. Safari hii niliweza kumuona yule msichana aliyejitambulisha kwa jina la Alice niliyekutana naye kule hotelini kwenye bwawa la kuogelea akiwa amavalia sare za kiaskari.
“Mr. Molito.... Kwanini ulitaka kujitia hatiani ili hali huusiki na hili tukio?”
Alice aliniuliza na kunifanya nimtazame usoni kwa mshangao kidogo.
Sura yangu ilitengeneza nuru baada ya kugundua kua askari hao wamechunguza kwa kina na kugundua kua sihusiki na tukio hilo la mauaji.
“nilikua nahofia mateso ya kurushwa na umeme au yale ya mateso mwanzo ya kukatwa vidole kwa msumeno na nyundo. Ndio maana nilikiri kua mimi ndio muhusika wa mauaji hayo kwa kutuma watu, Ila nia na madhumuni yangu ni kwenda kukana mashtaka hayo huko mahakamani.”
niliongea maneno hayo na kumfanya yule askari aliyekua ananihoji toka mwanzo aachie tabasamu.
“tumegundua waliyehusika na mauaji ni ya Farahani sio wavulana. Ni wasichana. Wapo watatu na muda wa tukio kufanyika ni baada ya wewe tu kuondoka kwenye nyumba ya marehemu. Inaelekea hao wasichana bila shaka kabisa unajuana nao. Maana walikua wanakufuatilia wewe kuanzia hapo hotelini mpaka wakafanikiwa kupajua nyumbani kwa Farahan na kumuua mfanya biashara huyo. Sasa sikiliza kwa umakini mkubwa, unatakiwa utusaidie ili tuweze kuwanasa hao wasichana. Hivyo tutakuachia lakini hutakiwi kutoka nje mji huu mpaka pale tutakapo wabaini wauaji na wewe kukupa ruhusa.” yule askari aliongea maneno hayo na kunifanya kidogo moyoni mwangu nifurahi. Maana kesi yangu hapo ni ndogo sana tofauti na ile ya mwanzo ya kuhisiwa ni muuaji wa moja kwa moja.
“tuliingia chumbani kwako na kupekua pekua kwa idhini ya muongozaji wa hoteli uliyofikia. Tuna passport yako na pesa zako zote zipo hapa. Hivyo unatakiwa ukubaliane na sisi kile ambacho tutahitaji ufanye ukiwa chini ya ulinzi wetu.”
Aliongeza askari huyo na kunifanya nikubaliane nao.
Niliambiwa sitakiwi kurudi tena kwenye hoteli ile, na badala yake nitaenda kukaa kwenye nyumba ya yule askari mpelelezi.
Nilianza maisha yangu rasmi ya upelelezi. Kwangu ilikua sawa na kifungo cha nje. Maana hata simu zangu tu zilirekodiwa kila ninapopiga na kupokea.
Nilitamani kutoa taarifa kwa familia yangu kwa majanga yaliyonikuta, ila nikashindwa kufanya hivyo kwakua sikua mkweli toka mwanzo. Na endapo ningeulizwa na mpenzi wangu kuhusu mikataba na wazungu niliyoenda huko Marekani kusaini ndo ingeniharibia kabisaa na kuwafanya askari hao kuwa na mashaka na mimi kwa uongo wangu. Nikaamua kunyamaza huku nikuomba kwa Mugu wangu ajaalie hao wahusika wakamatwe haraka ili na mimi niweze kurudi nyumbani.
Siku moja mishale ya saa mbili usiku kwa saa za Marekani, nilikua nimejipumzisha kitandani huku nikifuatilia taarifa mbalimbali za nyumbani kwetu Tanzania.
Kulikua na tukio kubwa la tuzo za waandishi wa riwaya na maishairi zinazoitwa tuzo za Mabati. Tuzo hizo zilikua zinawakusanya waandishi mbalimbali afrika mashariki na mimi nilishiriki shindano hilo. Mpenzi wangu nilimuagiza akaniwakilishe siku ya fainali kwakua nilikua nakiamini sana kitabu changu cha Siku 71. Hivyo kama matarajio yangu, niliibuka mshindi wa kwanza wa mashindano hayo kupitia kitabu changu hicho.
Nilifurahi tu kuiona tuzo yangu ikiwa kwenye mikono salama huku muhusika wa tuzo hiyo nikiwa chini ya uangalizi mkubwa wa kipelelezi japo kesi hainuhusu tena.
Baada ya kumaliza kufuatilia makabidhiano ya tuzo hizo. Nilizima data na kutoka chumbani kwangu hadi kwenye meza ya chakula.
Nilipomaliza kula nilirejea tena kitandani kwangu kw aajili ya kujipumzisha.
Huko niliweza kiona missed call kwenye simu yangu ya mtu nisiyemfahamu. Tena nimepigiwa kwa namba za hukohuko Marekani.
Niliamua kumpigia mtu huyo ili niweze kumjua ni nani hasa aliyenitafuta usiku huo. Maana hisia zangu ziliniambia kua huenda alikua amekosea namba.
“hello.”
nilipiga na sati ya kike ilisikika baada ya simu kupokelewa.
“hello,nani mwenzangu.” niliuliza baada ya kuisikia sauti hiyo.
Nilisikia cheko tu bila utambulisho. Ila cheko hilo liliweza kunijulisha ni nani aliyenipigia simu usiku huo.
“Haiba.”
Nililitaja jina hio lililomfanya msichana huyo akatishe kicheko chake.
“ndio mimi... Niambie Molito.”
Aliongea na kunifanya nikae vizuri. Hata kale kausingizi kalikokua kananinyemelea kote kaliruka na kunifanya nipate nguvu mpya ya kuongea na msichana huyo mtekaji mkubwa wa moyo wangu.
“safi... Hakika nimefurahia sana maamuzi yako ya kunitafuta tena... Na naomba unisamehe Haiba kwa kitendo changu cha kukuuliza maswali yaliyokukera kule kwenye mgahawa. Amini kua siwezi kurudia tena kukuuliza maswali ya kukukera.” nilijihami mwenyewe ili nisimpoteze tena msichana huyo.
“usijali... Naona bado upo Marekani unakula bata tu... Ni kwa sababu yangu au kuna vitu vingine unafanya?” Haiba aliuliza swali hilo.
“nipo kwa ajili yako mama... Hata hivyo nilishakata tamaa. nilikua nina mpango wa kuondoka na kurudi nyumbani, kama si kesho basi kesho kutwa.”
nilijibu huku nikijitahidi kuondoa waiwasi wangu. Maana nilikua najua fika kua maongezi hayo yalikua yanarekodiwa na wapelelezi wa kesi hiyo.
“nimefurahi kusikia hivyo... Nilikua najaribu tu kama namba yako itapatikana... Kesho nitakupigia ili tuweze kuonana.” Haiba aliongea maneno hayo na kunifanya nitabasamu.
“nitafurahi sana Haiba.”
nilijibu na Haiba akanitakia usiku mwema na kukata simu.
Asubuhi niliitwa na wapelelezi hao na kuulizwa maswali mawili matatu kuhusiana na msichana niliyekua naongea naye. Wakataka niwatafsirie pia maongezi yetu kwa kiingereza baada ya kunisikilizisha sauti zetu. Kwakua hakuna kibaya tulichokiongea, nilifanya hivyo kwa uwazi bila kubadili maana ya kila neno.
“kuwa huru kwenda kukutana nae. Ila tutakuwekea kifaa cha kurekodia sauti ili tuweze kusikiliza maongezi yenu. Hatuna maana kama tunamuhisi huyo rafiki yako ndio muuaji, Hii ni kwa usalama wako na usalama wa taifa kwa ujumla kuhusiana na wanawake hao hatari ambao bado hajuwajua mpaka hivi sasa.”
Kwakua nili ruhusiwa kuonana na Haiba, sikua na wasiwasi wowote. Nilikua najua maongezi yetu tutakayoongea hawatayaelewa mpaka mimi nitakaporudi kuwatafsiria. Mara zote ninapoonana na Haiba hua tunaongea kiswahili.
Mida ya saa sita mchana, nilipigiwa simu na Haiba. Niliipokea kwa shauku kubwa. Maana simu hiyo ndiyo niliyokua naisubiria wakati wote.
Aliniomba tuonane kwenye ule mgahawa tuliopishana kauli mara ya mwisho baada ya dakika ishirini. Nilienda kujiandaa haraka na kuwahi eneo la tukio.
Kwakua nilipokua naishi si mbali sana na mgahawa huo ulipo, ilinichukua robo saa kujiandaa na kufika hapo.
Nilichagua eneo ambalo nilihisi litakua tulivu muda wote. Baada ya dakika kumi, nilimuona Haiba akiingia na kuangaza macho yake kushoto kulia kuashiria alikua akinitafuta. Baada ya kuniona alinisogelea huku uso wake ukijawa tabasamu.
Hakika Haiba alikua na upekee kila nimuangaliapo. Haijalishi nitakutana na wasichana wangapi na kwa muda gani. Ila nikikutana na Haiba hua nahisi kabisa nimekutana na kiumbe tofauti kabisa. Nadhani kwa vile moyo wangu umekwama kwake.
“habari za toka siku ile.”
Haiba aliongea huku tabasamu likitamalaki kwenye uso wake.
“salama tu... Hakika nimefurahi sana kunitafuta kwako. Nilikua nadhani kua ule ndio mwisho wetu wa mimi na wewe kuonana tena kwa vile ulivyoondoka ukiwa umenikasirikia.” niliiongea hofu yangu dhahiri na kumfanya Haiba acheke na kujiinamia kidogo kwa aibu kisha akainua uso wake na kunitazama machoni.
“wala usijali Molito, mimi mwenyewe nilijisikia vibaya nilipokua nyumbani kwangu na kuwaza vile nilivyotenda juu yako. Hakika nilijiona mkosaji. Ndio maana niliamua kukupigia baada ya kuhisi huenda uliumia moyo na kupoteza hamu ya kuonana na mimi tena.... Nilipoona bado una hamu ya kuwa na mimi karibu, nikapata hata nguvu za kukuita hapa.” Haiba aliongea na kunifanya niachie tabsamu.
“Leo una ratiba gani?”
Haiba aliniuliza na kunifanya nimuangalie haraka usoni na kumjibu.
“sina ratiba yoyote ile... Nipo tu.” nilimjibu na kumfanya anitazame huku akiwa ameyalegeza macho yake mazuri yaliyonipa umakini wa kutaka kusikia kitu kinachofuata. .
“nataka unisindikize mahali kama hutojali.”
Haiba aliongea maneno hayo na kunitazama usoni.
“wewe tu, ila mimi sio mwenyeji huku ndio maana nimeshindwa hata kukuuliza nikusindikize wapi.” niliongea na kumtazama Haiba huku na mimi nikijitahidi kutabasamu ili mradi kulifikia tabasamu la Haiba ambalo alikua ananipatia bila kulibania.
Kila muda hata kwa maongezi yasiyochekesha, uso wake ulionyesha wazi kuyafurahia maongezi yetu.
“ni nje kidogo ya mji huu.... ni jirani na hapa, mji huo unaitwa Philadelphia .... Ni mwendo wa dakika arobaini na tano tu kwa treni.” Haiba aliongea maneno hayo na kunitazama. Hakika nilishtuka kidogo. Maana mji huo ndio mji ulionipatia majanga na kunifanya niendelee kubaki hapo Marekani lakini si kwakupenda. Nipo chini ya uangaliazi wa askari na hapo nilipo nilikua na vifaa mwilini mwangu vilivyokua vinawafanya wanifuatilie kila hatua ninayopiga.
“sawa.... Tunaenda lini?” niliamua kumuuliza.
“muda huu.. Nilihofia kukwambia ukiwa mbali kwa kuhisi utanikatalia ndio maana nikasubiri uje kwanza niongee na wewe ana kwa ana.”
Maneno ya Haiba yaliniweka kwenye utata mkubwa. Maana siruhusiwi kutoka nje ya mji huo kutokana na kesi ya mauaji ya mfanya biashara Farahan niliyohusishwa nayo.
Mara ujumbe mfupi wa maandishi ukaingia kwenye simu yangu.
“nenda popote pale anapokuambia.”
Ujumbe mfupi niliotumiwa ulisomeka hivyo ukiwa umetumwa kwa lugha ya kiingereza. Hapo nilipata mshtuko mwengine ambao ulimfanya mpaka Haiba ahisi nimepokea habari mbaya kwenye simu yangu muda huo. Nilijitahidi kuua soo kwa kutabasamu kwanza na baadae kushangilia.
“umekua mshindi kwenye bahati nasibu?” Haiba aliuliza baada ya kusoma alama zote mbili nilizozionyesha za mishtuko.
Kwanza mshtuko ule wa kwanza kabisa wa hofu na mwengine ni furaha liyojitengeneza ghafla kwenye muonekano wangu wa uso.
“nimeshinda tuzo nyingine huko Tanzania. Ndio ujumbe wa kunipongeza umeingia hapa. Yaani hata sikua na habari kama jana ndio ilikua fainali.”
Nilimjibu hivyo ili kuweza kuua ile hali iliyonitokea ghafla. Ila kiuweli kabisa kilichonishtua ni vile wapelelezi wa nchi hiyo walivyokua wanafautilia maongezi yetu na kuelewa kila kitu tulichokua tunaongea wakati tumetumia lugha ya kiswahili.
“hongera sana Molito kwa tuzo nyingine. Unazidi kunidhihirishia wewe ni muandishi mkubwa kiasi gani... Vipi, kitabu changu umekuja nacho?” Haiba aliuliza baada ya kukumbuka ile ahadi yangu niliyomuahidi siku ya kwanza kuonana naye.
“ndio.” nilimjibu na kumfanya afurahi sana.
“nakiomba jamani.” aliniambia hivyo na mimi nikafungua begi langu dogo nililoenda nalo na kutoa kile kitabu nilichokipiga sahihi yangu kabisa na kumpatia mrembo huyo.
Haiba alikipokea kitabu hicho kwa furaha na kufungua kurasa ya kwanza. Aliona sahihi yangu ikiwa na jina lake kabisa ,niliweza kugundua vile alivyokua anajisikia muda, alisimama.
“molito, naomba nikukumbatie.”
Kauli hiyo ilipenya haraka kwenye ngoma za masikio yangu na mwili ukawa na haraka ya kunyanyuka kabla sijajibu kitu chochote na kumfanya Haiba aelewe kua nimenyanyuka kwa ajili ya kupokea kumbatio lake.
Alinivamia na kunikumbatia. Hakika mwili wa Haiba ulikua ni mwili fulani hivi wenye joto tamu. Nilitamani niendelee kumkumbatia tu na kile kibaridi kilichokua muda huo ndio kabsa, nilisisimkwa mwili mzima.
“Ahsante sana kwa zawadi hii.... Hakika sijawahi kupata rafiki bora kwenye maisha yangu kama wewe.” Haiba alitamka maneno hayo akiwa kwenye kumbatio langu.
“hata mimi sijui niseme nini.... Ila hua ninafurahi niwapo karibu na wewe.” nilijikuta na mimi nimeongea maneno hayo na kumfanya Haiba atoke kwenye kumbatio langu na kunitazama.
“Twende Molito... Treni inakaribia kuondoka.”
Haiba aliongea maneno hayo baada ya kuangalia saa yake. Na mimi bila kuhoji chochote, niliamua kwenda huko anaponipeleka Haiba. Wala sikua na hofu ya kitu chochote kwakua niliamini mtu ninayempenda hawezi kunidhuru.
Basi tukaianza safari kuelekea kwenye kituo cha treni. Tulifika huko na kuingia kwenye usafiri huo ambao ulitupeleka hadi kwenye mji wa Philadelphia.
Tulichukua usafiri wa jumuiya mwengine na kutupeleka kwenye mitaa ambayo kumbukumbu zangu ziliniambia kua hatukuwahi kuipita wakati nazungushwa mji huo na familia ya marehemu Farahani.
Tulifika kwenye nyumba moja ndogo ya mbao tupu lakini iliyojengwa kwa ustadi mkubwa na kuingia ndani yake.
“karibu Molito... Hapa ndipo nyumbani kwangu. Hivyo jisikie huru.”
“nashukuru sana... Nimeshakaribia.”
“ nilipokuambia kua nakaa mbali nilikua namaanisha... Kama unakumbuka siku ile tulipokutana kwa mara ya kwanza kule mgahawani.”
Haiba aliongea na kunifanya niangalie mazingira ya nyumba ile kwa ndani. Sebuleni palijaa fremu zilizokua na picha zake. Na fremu zingine akiwa na mama wa Kimarekani.
Kwa mazingira yake tu,niliweza kuamini kua kweli hapo ndipo mahali anapoishi Haiba. Ila kutoona picha za mwanaume yeyote yule wala wazazi wake halisi, niliweza kuamini kua ni kweli Haiba hakua anakumbuka kitu chochote na wala hana tena kumbukumbu za wazazi wake waliomzaa.
Nilikaa kwenye moja ya masofa na kumsikilizia mwenyeji wangu.
“nikupatie kinywaji gani?” Haiba aliniuliza.
“nipatie Juisi halisi ya embe kama ipo.”Niliuliza na kumfanya Haiba atabasamu.
“Ngoja niitengeneze dakika chache tu hapa. Maana matunda yapo ya kutosha.”
Kauli ya Haiba iliendana na kitendo. Alienda jikoni na baada ya dakika tano alirudi na glasi mbili zilizojaa juisi za matunda hayo.
“karibu sana mwandishi mkubwa kutokea nchini Tanzania. Nadhani leo sitalala, nitakisoma kitabu hiki mpaka nikimalize.” Haiba aliongea baada ya kukitoa kitabu cha Siku 71 kutoka kwenye begi lake na kunifanya na mimi nitabasamu.
“Umemuona mama yangu?” Haiba aliuliza na kunitazama. Niliangaza kulia na kushoto. Nilihisi huenda alikua chumbani ndio amefika hapo. Kumbe alikua ananionyeshea ukutani ambapo pana picha ya mama mwenye ngozi nyeupe.
“nimemuona.... Ila bila shaka ni mama yako mlezi.” niliongea maneno hayo baada ya kuona yeye na mama huyo wa Kimarekani hawafanani hata kidogo.
“umejuaje?” Haiba aliuliza huku anacheka.
“wewe una sura nyembamba halafu ndefu. Yule mama pale ana sura ya duara. Halafu wewe haujakaa kwenye asili yake. Mpo tofauti sana.” nilijibu na kumfanya Haiba atabasamu na kunywa kinywaji chake.
“ni kweli kabisa.... Huyu mama aliniokota nikiwa sijitambui baada ya kupata ajali ile niliyokueleza iliyopoteza uhai wazazi wangu. Akanipeleka hospitali na kunihudumia hadi nimekua Haiba tena huyu unayemuona hivi sasa. Japo kumbukumbu zangu bado hazijarudi sawasawa, ila namshukuru sana kwa kunisimamia vyema kama mtoto wake wa kumzaa kwa kipindi chote cha matibabu yangu.”
Haiba aliongea maneno hayo yaliyo nishawishi kujua mama huyo kwenye picha ana moyo mzuri kiasi gani.
“unaishi naye au yeye anaishi kwengine?” nilimuuliza baada ya kuhisi huenda Haiba anaishi peke yake humo.
“ni hadithi ndefu kidogo... Ila hayupo hai kwa sasa.” Haiba aliongea kwa masikitiko na kunifanya hata mimi niingiwe na imani.
“pole sana kwa yaliyokukuta.”
Nilimpooza na kunifanya nitazame tena picha ya mama huyo. Nilimuombea kimoyo moyo Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
“nimekuleta huku ili unisaidie Molito.... Naomba unikumbushe vitu vyote unavyovijua kuhusu mimi ili nijijue mimi ni nani. Kama unawakumbuka wazazi wangu niambie wapoje. Kama unapajua nyumbani, nipo radhi tuondoke wote ili nikapaone. Huenda kukawa na picha zao au kitu chochote cha kunikumbusha kuhusu wao. Hakika wewe ni msaada pekee kwangu uliyebakia ambaye naamini naweza rudisha kumbukumbu zangu za awali kabla ya ajali kutokea.” Haiba aliongea maneno hayo huku akionyesha wazi kua na kiu ya kutaka kumbukumbu zake zirudi.
“hata sijui nianzie wapi Haiba kukuelezea vile ninavyo kufahamu.. Ila kifupi tu, mimi sikuwahi kuwaona wazazi wako na wala sijui wanafananaje. Ila mimi na wewe tulionana muda mrefu sana uliopita. Yapata miaka nane mpaka tisa toka tumeonana. Kipindi hicho ulikua unasoma kidato cha pili. Ulikua unamiliki laptop ambayo ilipata hitilafu ya kuungua kioo. Ulikuja ofisini kwangu na mimi nikakupatia ufumbuzi wa kifaa chako. Ulilipa kiasi nilichokuambia na kifaa chako kikapona na kuwa kizima kama awali. Hapo ndipo tulipoanza urafiki wetu. Ukanifungulia akaunti ya facebook. Hata email ninayoitumia ni wewe ndio umenifungulia. Mazoea yakatengeneza penzi kwenye moyo wangu. Mapenzi ya ajabu ambayo sikuwahi kuyawaza hapo kabla. Kiukweli nilijikuta naumia sana kukaa na siri ya kukupenda bila kusema. Wakati tunakutana mimi nilikua nasubiri majibu yangu ya kidato cha nne. Niliendelea na kidato cha tano na sita na hapo tukawa tunaonana kipindi cha likizo tu. Wewe ulipomaliza kidato cha nne ukafaulu kuendelea na ngazi inayofuata. Nakumbuka niliporudi nilijipanga kabisa kuongea na wewe kwakua ulishakua mtu mzima na bado ulionyesha wazi kua ulikua unanipenda, sema ulikua unanisubiri nianze kusema. Nilikupa mwaliko na kukutana na wewe kwenye hotel ya Kunduchi beach na kukuambia vile nakupenda. Uliniambia nikupe muda ujifikirie. Ndipo siku moja ukanipigia simu usiku na kuniambia kua una mtu wako na mnapendana sana. Hutaki kumpoteza hivyo mimi na wewe mahusiano yetu yakomee hapo. Hata urafiki wa kawaida tu hutaki kwakua utakusababishia kutengana na mtu wako. Ulikata simu bila kunisikiliza na kunifungia kabisa mawasiliano yangu na yako. Toka siku hiyo sikukutafuta tena. Niliheshimu maamuzi yako japo niliumia sana kwenye moyo wangu. Nikaanza kuhangaika na wanawake mbalimbali ili niweze kuuziba pengo lako. Lakini bado Haiba alibaki kuwa Haiba tu. Sikuweza kumpata mwanamke mwengine kama wewe. Sikuweza kupata mwanamke wa kudumu naye hata kwa miezi mitatu. Sikuchagua wanawake wa kutembea nao, nilikua nagusa Msichana yeyote yule hadi nilipomtia mimba mtoto wa watu na kulazimika kuishi naye baada ya wazazi wake kuja juu. Na mwanamke ambaye nimezaa naye ni yule ambaye uliniona naye siku ile. Hata hivyo dhiki zilipozidi alinikimbia na kuniachia mtoto. Nami nikampeleka mtoto kwa mama yangu. Alinikimbia kwakua hata yeye hakuwa tayari kuishi maisha magumu niliyokua nayapitia kipindi hicho. Ndipo nilipoanza kuandika riwaya kwa uchungu na hisia kali. Mungu akanijaalia baada ya miaka kadhaa ya mateso nikashinda tuzo hiyo iliyobadilisha maisha yangu kifedha na kunikutanisha tena wewe huku Marekani. Kwa bahati mbaya sikukutana na yule Haiba wangu nimpendaye, Nimekutana na Haiba mwengine kabisa. Haiba ambaye hana kumbukumbu hata moja kuhusu mimi..... Nadhani hivyo ndivyo ninavyoweza kukukumbusha Haiba.”
Baada ya kumaliza kuongea maneno hayo, nilimuangalia Haiba. Nilimuona akibubujikwa machozi. Hakika hadithi yetu ilikua inaniumiza hata mimi msimuliaji. Maana sikuwa nalia lakini macho yalishaiva na kuwa mekundu kwa uchungu wa kumkosa mwanamke niliyevutiwa naye kwenye maisha yangu.
“naomba unisamehe sana Molito... Sikumbuki chochote kile kati ya hivyo ulivyo ongea. Ila nimeumia sana baada ya kunihadithia yote hayo yanayohusu hisia kali za mapenzi ulizo nazo juu yangu... Labda nikuulize swali kabla na mimi sijaongea kitu chochote na wewe. Kwani bado unanipenda mpaka hivi sasa?” Haiba aliuliza swali hilo na kunitazama usoni.
Nilijikuta nimesisimkwa mwili kwa swali lake. Nilipomuangalia, niliweza kugundua macho yake yalikua yanamaanisha juu ya umuhimu wa jibu langu kwa swali aliloniuliza.
ITAENDELEA.............
Thursday, April 25, 2019
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Write comments