Pages

Monday, May 20, 2019

Maneno makuu ya kimapenzi yenye thamani kwa mwanamke

KATIKA uhusiano wa kimapenzi yapo maneno mawili yenye thamani kubwa na yenye kubeba ujumbe mzito wa kimapenzi kwa mpenzi umpendaye kwa dhati, maneno hayo ni, 'nakupenda' na 'nitakuoa'.

Maneno haya mawili kwa wenye kujua thamani yake si rahisi kuyatamka ovyovyo kwa yeyote yule asiye na mpango naye wa kumpenda wala kumuoa.

Kutamka maneno hayo kwa hitaji la kumlaghai mpenzi ama mchepuko katika kumpata kimapenzi ni uhuni na tena ni dhambi kubwa.

Cha kushangaza mara nyingi tumekuwa tukishuhudia ama kuona wapenzi wengi wakisimulia au kuelezea kwa namna alivyoweza kulaghaiwa na kuumizwa moyo na mtu aliyedhani kuwa kweli angeweza kumpenda kutoka moyoni mwake na kumuoa.

Utaona huyo akisimulia kwa namna alivyoweza kukutana kwa mara ya kwanza na mchepuko huyo aidha kwa njia ya kuonana naye ana kwa ana, kwa njia za mitandao ya kijamii ama kwa njia ya mawasiliano ya simu.

Kuonana huko ndiko kulikomsababisha apagawe, achanganyikiwe, alainike na kuingia mtegoni kwa maneno matamu aliyoyasikia masikioni mwake. Masikini! kumbe ni uongo mtupu, huku kwa upande wake akiambulia kujiuliza kama anapendwa kweli.

Bila shaka kwa mwenye kulitaka lake jibu huwa ni rahisi sana, nakupenda. Wapo pia wale wanaotanguliza neno hilo pasipo hata kuulizwa.

Hiyo yote ni katika kujaribu kuuteka moyo wa yule anayemtamani kimapenzi ili aweze kumuaminisha kuwa napendwa lakini pia kupata uhakika wa uwezekano wa kuoa au kuolewa.

Ni katika hali ya namna hiyo, wengi wamekuwa wakidanganywa na kuachwa solemba. Lakini kama wangeweza kujua kuwa, suala la kupenda, kuoa au kuolewa lina thamani ya pekee katika maisha ya watu wenye mapenzi ya dhati asingeweza kutamka maneno hayo kwa asiyempenda.

Kwa jinsi hiyo, kwa anayejua maana na umuhimu wa maneno hayo si rahisi mara moja kukubaliana na mpenzi wa aina hiyo.

Lakini pia kwa mwenye mapenzi ya kulaghai na asiyependa kutamka maneno hayo badala yake utaona akitafuta namna au mbinu nyingine ya kumnasa mchepuko huyo.

Aina ya maneno atakayotumia kama hatakuwa makini katika kuujua ukweli ama uongo wake, yanaweza kukuteka kisaikolojia na pia kukusababisha uweze kweli kuamini maneno hayo.

Kwa mfano, mpenzi anaweza kukutamkia kuwa, "usiwe na wasiwasi kuhusu hilo, ni vizuri kwanza tujuane, halafau wewe mwenyewe upime kama kweli nakupenda au la.

“Halafu kuhusu suala la mimi na wewe kuoana hilo ni matokeo ya hatua kwa hatua. Kwa maana nyingine si jambo la kukurupuka. Sitaki uone kama nakudanganya, nataka uniamini kuwa mimi ni mkweli na hata nitakapokutamkia nakupenda uone kweli imetoka moyoni mwangu"

Aina ya uongeaji wa namna hiyo ni katika kumpoteza mpenzi ama mchepuko kwa lengo la kumpata kimapenzi.

Mpenzi huyo atakapoingiwa na tamaa kwa kuamini maneno hayo kwa haraka pasipo kuchukua muda mrefu wa kuyatathmini na kuyafanyia kazi maneno hayo ni rahisi kuingia kichwa kichwa kulaghaiwa kiulaini na baadaye kuumizwa moyo wake.

Pia kumbuka kwamba, anapotamkiwa mchepuko maneno ya aina hiyo, iwe kwa njia ya kuonana ana kwa ana, kwa njia ya mitandao ya kijamii au kwa njia ya simu kwamba, 'nakupenda sana' na pia ikibidi kwa kuongeza kutoa ahadi ya kumuoa huku akijua fika hana nia naye, ni kumsaliti mpenzi, mchumba, mke ama mume wako.

Aidha, utumiaji wa maneno 'nakupenda na nitakuoa' bila kujali thamani ya maneno hayo ni kumuumiza mpenzi au mchepuko huyo moyo wake.

Pia kumsababisha aumie kisaikolojia, kutafuta njia ya kujiua kwa sababu tu ya kushindwa kuamini kwa kile kilichotokea baada ya kusikia kuwa maneno uliyomtamkia ni katika kuhitaji kumpata kimapenzi.

Kwa jinsi nyingine, utumiaji wa maneno hayo yanaweza kukusababisha yakushushie thamani ya mapenzi baina yako na yule unayependa kwa dhati.

Wakati mwingine utumiaji wa maneno hayo hayo yanaweza kumsababisha yule uliye na lengo naye la kumlaghai kimapenzi akuroge, aidha kwa nia njema ya kukupata kimapenzi baada ya wewe kumuongopea ama kukuroga kwa nia mbaya ya kukuumiza na wewe moyo wako.

Wakati mwingine kabla ya kutamka maneno hayo, ni vyema mpenzi akajiuliza mara mbili mbili kwa kile anachotaka kufanya kwa yule aliye na lengo naye la kumdanganya.

Ajiulize kwamba, je, ni sahihi kumwambia mtu mwingine tofauti na uliyemchagua moyoni mwako, ukampenda kwa dhati yako na pengine hata kumchumbia na kufunga naye ndoa kuwa unampenda na utamuoa mtu mwingine tofauti na yeye?

Hebu ukiwa kama mpenzi na una mchumba, mume ama mke jaribu kubadilika tabia yako kwa kutunza heshima ya penzi la mwenzi wako, ikiwa kama yeye ana kuheshimu na kukutunzia mapenzi yenu, kuwa na hofu ya Mungu ndani yako.

Lakini pia kuwa mkweli kwa maneno unayotamka. Usifanye jambo au kutamka maneno matamu kwa hitaji la kumridhisha kumpata unayemtaka kimapenzi.

Usitumie maneno nakupenda kwa usiyempenda, na wala usimuahidi kuwa utamuoa, haipendezi.

No comments:
Write comments

Recommended Posts × +