Kupendwa kwa vitendo
Tulishaona kuwa hadhi ya mwanaume inategemea kwa kiasi kikubwa namna anavyoheshimiwa. Kwa mwanamke hali ni tofauti. Hadhi yake inategemea namna anavyopendwa na mwenzi wake.
Upendo kwa mwanamke unaeleweka anapoambiwa bila kuchoka na kuthibitishiwa kwa kutendewa vitendo kuwa anapendwa. Katika lugha ya kiingereza, hapa tungetumia neno affection, yaani matendo yanayoonesha mapenzi kwake.
Hata hivyo, lugha ya mapenzi hutegemea mambo mengi. Kuna athari za utamaduni, desturi na imani zilizopo katika jamii aliyokulia mwanamke. Hata hivyo, yapo matendo yaliyothibitika kuvuka mipaka ya kiutamaduni.
Mfano, kumwambia mwanamke unampenda mara nyingi iwezekanavyo, ni hitaji la msingi. Kwa mwanamume, kuambiwa anapendwa inaweza isiwe jambo la maana, lakini si kwa mwanamke.
Mwanamke anatamani kusikia mara nyingi kadri inavyowezekana kuwa anapendwa.
Pia kuna vitu kama kupewa zawadi asizotarajia, kutumia muda wa mapumziko pamoja nae, kutoka naye kwenda mbali na nyumbani na mambo kama hayo yanayoonesha kuwa kweli unampenda.
Ndio kusema, ikiwa unataka kuugusa moyo wa mwanamke, akupe heshima unayoihitaji kama mwanaume, unawajibika kujua vitu gani mahususi ukimfanyia vinatuma ujumbe wa wazi kuwa unampenda. Usipoweza kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, anapoteza hamu ya uhusiano.
Huchoka kihisia na anaweza kufanya mambo yasiyotarajiwa ili tu kuhujumu mahusiano.
Anataka kuwa kipaumbele chako
Mwanamke hapendi kujikuta katika mazingira ya kushindania nafasi ya kwanza na kitu kingine chochote iwe ni kazi, mtu au chochote kile unachokipenda wewe mwanamume.
Tulishaona kuwa kwa mwanaume, hadhi yake hutegemea zaidi namna uwezo wake unavyotambuliwa. Hali hiyo humfanya mwanamume atumie muda mwingi kufanya mambo yanaweza kumpa heshima katika jamii. Inaweza kuwa kazi, biashara, mamlaka na namna zozote zile zinazomwongezea uwezo.
Lakini wakati anapotumia muda mwingi katika mambo hayo, ni rahisi kuonekana ameyafanya mambo mengine kuwa ya muhimu kuliko uhusiano wake na mwenzi wake. Wanawake wengi hawapendi kujikuta katika hali hii. Hapa ndiko iliko tofauti.
Mwanamke hatamani kuwa kwenye nafasi ya ‘mengineyo’, ‘ziada’, ‘baadae’ ‘nikipata muda’. Unapomweka ‘akiba’ mwanamke hawezi kufurahia kwa sababu anatamani awe kipaumbele chako.
Mambo mengi huthibitisha kuwa umempa nafasi ya kwanza. Mfano kuwa na muda wa kuwa naye mara nyingi kadri inavyowezekana, kuahirisha mambo mengine ya muhimu kwa ajili yake, kuwahi miadi unapoahidi kukutana nae, kuwasiliana naye kwa karibu na mambo kama hayo. Unaposhindwa kufanya hivyo, mwanamke hupata ujumbe kuwa yeye ni mtu wa ziada baada ya mambo ya muhimu.
Kadhalika, ili kumwambia yeye ni kipaumbele, mwanamke anatamani kila unapoongea nae akili yako yote iko pamoja naye. Kuwa pamoja naye maana yake ni kuachana na vyote vinavyokuondolea uzingativu na kumsikiliza kwa makini.
Mwanamke anatamani unapozungumza naye ufuatilie anachokisema, umpe mrejesho kuwa unamwelewa na uonesha kuwa mwili, akili, hisia ziko pamoja naye kumsikiliza. Vinginevyo, mwanamke anakuoana kama hujaweza kumpa nafasi yake anayoistahili.
Friday, May 24, 2019
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Write comments