Pages

Thursday, May 23, 2019

Ukijichanganya kwenye mapenzi, utapoteza mwelekeo wa maisha

Unaweza kuona ni kama swali la kipuuzi lakini lazima lipate jibu. Katika uchunguzi wangu kuna kitu ambacho nimekigundua, katika mapenzi ya sasa hivi eti wanajiita kwenda na wakati (dot com). Kumekuwa na tabia ya kukosekana kwa uaminifu, watu wamekuwa wakizungukana, hata marafiki.

Hii imekuwa ikiwakuta wasichana wengi hasa wanafunzi ambao wamekuwa wakiingia katika mapenzi bila kujua nini hasa maana ya mapenzi. Wengi wao huona kuwa na mpenzi ni fasheni, kumbe mapenzi ni maisha kamili, ambayo kama utafanya vibaya huenda ukavuruka mpangilio wako wote wa maisha yako.

Nia yangu kubwa si kuwagusa wanafunzi ambao wamekuwa ndiyo wanaongoza kwa kuuliza maswali juu ya penzi lao kukosa muelekeo. Naomba twende pamoja ili tujue njia ya mapenzi ni ipi ambayo siku zote itakufanya uwe na penzi salama.


Siku zote unapoanza mapenzi hakikisha yule unayetaka kumkabidhi dhamana ya moyo na mwili wako yupo vipi. Usikurupuke kwa vile umeambiwa unapendwa, kuutoa mwili wako kwa mtu si jambo la mzaha hata kidogo.

Chukua muda wako kupata undani wa mtu anayetaka kuuhifadhi moyo wako, kwani kosa lako linaweza kukutia kwenye mateso makubwa. Japo kumjua mpenzi wa kweli yahitaji kutumia muda mrefu, lakini ni vizuri kuvuta subra kabla hujatoa uamuzi.

Pia unapokuwa umeanzisha uhusiano jiepushe kuchanganya wapenzi, anaweza kutokea mtu ambaye hakika moyo wake ulikuwa radhi kufanya lolote hata kuachika kwa ajili yako. Lakini bahati mbaya umo ndani ya ndoa au ndani ya penzi miliki.

Mapenzi yana njia moja, penzi la kweli ni lile ulilomo na wala si la pembeni. Sawa na mashindano ya riadha ya mita 100, ukikimbia katika mstari wa mwenzako utakuwa umefanya makosa.
Mwenzako akigundua hilo, huo ndiyo utakuwa mwanzo kutafuta njia ya kukuacha.

Makala haya yanawagusa watu wote walio kwenye ulimwengu wa mapenzi ili kujenga uhusiano ulio imara. Jiepushe kujirahisi hovyo, si kwamba unapendwa bali unajishushia heshima yako.

No comments:
Write comments

Recommended Posts × +