Pages

Tuesday, May 21, 2019

WHAT IS LOVE?

WHAT IS LOVE?


******
Umuhimu wake ulikuwa kama maji mwilini,sikutaka kuamini kama watu huwa wanapenda kama mimi nilivyompenda yeye.Siwezi kusema alikuwa moyoni mwangu,nahisi alikuwa ndio moyo wangu.Mapigo yangu ya moyo,furaha yangu wakati wote.Watu husema kuwa ukipendwa ndio raha lakini kauli hii niliamini haina ukweli wowote,ukweli ni kwamba ukipenda ndio raha,jinsi nilivyokuwa nikijisikia nikiwa na yeye sidhani kama mtu aliyependwa angejisikia hivyo.Ukiona mtu ameoa au ameolewa kwasababu tu amependwa pasipo yeye kupenda,basi ndoa hiyo haitadumu.

Upendo niliokuwa nao juu yake haukuwa wa kawaida,sidhani kama yeye alinipenda sawa na mimi nilivyompenda.Familia yetu ilikuwa ya kitajiri sana,walikuwepo wanaume wenye pesa lakini hawakufanikiwa kuuteka moyo wangu kama huyu mwanaume aliyetokea katika familia ya hali duni.Nilipomaliza chuo kikuu Uingereza,kurudi nyumbani nilikuta mabadiliko makubwa ambayo dalili zake nilianza kuziona wakati nikiwa uingereza,sikutaka kuziwekea maanani kwasababu Nilimpenda sana,
“Gibson una mke?” nilishtuka sana aliponiambia ameoa
“ni wazazi wangu walinishinikiza sio kwa kupenda kwangu,” alinijibu huku akiweka sura ya huruma.Nilijua anaigiza tu
“kwahiyo…” nilijikuta nikishindwa kuongeza neno lingine baada ya hilo na kuanza kulia.Sikuamini Gibson wangu amepotea kwenye maisha yangu ya baadaye yaliyokuwa na uzuri wake wa kufikirika.Niliondoka nikiwa na hasira sana,zilipopita siku tatu nikiwa nimeapa kutomtafuta tena…moyo ulishindwa,nikampigia simu na kumwomba hata niwe mke wake wa pili,aliniambia dini hairuhusu.Maisha nilianza kuyaonja katika upande wa chungu,wazazi wangu walijitahidi sana kuwa karibu na mimi katika kipindi hiko.Namshukuru Mungu sikuchanganyikiwa na kuwa chizi japo kuna muda sikujielewa kabisa kila nikiwaza kuwa Gibson sio wangu na hatokuwa wangu milele,
“nikafanye fujo kwenye harusi yake? Au nimteke aishi na mimi kwa lazima?” yote yalikuwa ni mawazo yangu ambapo baadaye nilijua ni hasira tu.Harusi yake ilikaribia ambapo kabla ya kwenda kushuhudia kipenzi changu anavyofunga ndoa na mwingine,nilisali Mungu anipe nguvu.Nilikwenda na niliwapa zawadi ya biblia,kuna wakati nilimwangalia huyo msichana kwa hasira,nilijiuliza ana nini mpaka ameweza kumchukua Gibson wangu.Harusi ilipoisha nilirejea nyumbani na kupumzika.

Ilipita miaka sita nikiwa sina hamu na mwanaume yeyote,moyoni mwangu bado aliishi Gibson wakati yeye alikuwa na furaha na mke wake.Walijaaliwa kupata watoto wawili wa kike ambao ni mapacha.Walipouanza mwaka wa saba wa ndoa yao,andiko la Mungu lilibidi kutimia.Walipata ajali ya gari,walikuwa familia nzima.Gibson,mkewe na watoto wake,Gibson na mkewe hawakuomba hata maji,palepale walifariki dunia.Basi walilopatia ajali lilikuwa ni kubwa na watu walijazana mpaka wengine kusimama.Watoto wao hao mapacha Vaileti na Valeria waliumia vibaya sana,wakati huo walikuwa na umri wa miaka mitatu.Nilipopata taarifa hizo niliumia mno kwani bado nilimpenda Gibson.

Uwezo wa kulipia matibabu kwa familia zote mbili hawakuwa nao hivyo niliamua kuingilia kati suala hilo.Sikutaka kuwaweka katika mizani kwamba ndio waliomshinikiza Gibson kuoa mwanamke mwingine wakati walijua yuko na mimi,wala sikutaka kusikia maneno ya watu kuwa wazazi wa Gibson ni washirikina na walitumia huo ushirikina kumshawishi mtoto wao aoe mwanamke mwingine ili mambo yao yaende vyema.Niligharamikia matibabu ambapo majeraha waliyonayo iliwalazimu kupumzishwa Hospitari kwa muda mrefu sana.Ajali hiyo ya basi ilikuwa ni msiba wa taifa zima,mapacha hao wawili ndio walifanikiwa kutoka salama lakini waliosalia wote walipoteza maisha,wengi palepale na wachache baada ya kufikishwa hospitarini.Watoto wazuri mapacha,wengi waliwaombea sana Mungu awaponye.

Baada ya kupelekwa mpaka nje ya nchi,ndio walipata ahueni,niliwalea kama watoto wangu,niliwasomesha na kuwajali kwa kila kitu.Wazazi wa Gibson walijishtukia na kuniomba msamaha kwa walichokifanya nikawasamehe kwasababu kosa halikuwa lao ni la mtoto wao,angenipenda angenisubiri badala ya kukubali kuoa mwanamke mwingine.

*****

“wanangu mbona mnalia jamani,kuna nini mnanitisha!” niliuliza kwa mshangao baada ya kuwakuta wamekaa chumbani kwangu kitandani wakilia.Wote wawili Valeria na Vaileti walikuja na kunikumbatia,bado sikuwalewa wamepatwa na nini
“mbona siwaelewi jamani watoto wangu,”
“ahsante sana mama,hatukujua uliyoyapitia,”
“Ahsante mama,tunakupenda mama yetu.” Vaileti na Valeria waliniambia hivyo na kunitisha sana,ila nilipotupia macho yangu kitandani niliiona 'Diary' yangu niliyoandika historia kuhusiana na Gibson mpaka kuwaokoa watoto hao.Niliiandika muda mrefu kidogo kama miaka ishirini na tatu iliyopita.Vaileti na Valeria walikuwa ni mabinti wakubwa kabisa,niliwapeleka chuo kikuu uingereza na walikuwa mwaka wa pili.Basi ikabidi niwakumbatie pia na kuwaelewesha vizuri,waliniona mtu wa ajabu sana kwani mpaka muda huo sikuwa na mpango wa kuolewa na nilikuwa na miaka thelethini na moja,nilizidi kuwaambia baba yao ndio mume wangu wa maisha,anaishi moyoni mwangu milele yote.Hakuna mtu anayeweza kuwa na mimi zaidi yake.Vailet na Valeria walijifunza kitu kikubwa sana siku hiyo kuhusu Upendo,
“kwahiyo hutakuja kuolewa?” alihoji Vaileti.
“sina mpango huo,hata umri nao umeshasogea.”
Kitu kingine kilichonipa furaha nikiwa nao,walifanana sana na baba yao Gibson.Muda mwingi nilicheza nao kama wote ni watoto wadogo ambapo tulijisikia amani sana.
Upendo hauhesabu mabaya,
Upendo huvumilia.

MWISHO.

No comments:
Write comments

Recommended Posts × +