Pages

Friday, May 24, 2019

MKASA WA MAPENZI: RIPOTI KAMILI

Jifunze kuwa mwisho wa jambo moja ndio mwanzo wa jambo jingine. Linaweza kuisha jambo baya likapokelewa na jambo jingine baya zaidi ama linaweza kuisha jambo baya na kupokelewa na jambo jema……

Na hii ni sehemu ya kumi na nne

Ninachokumbuka kuwa nilikuwa napiga ngumi huku nikitukana, kila ngumi ilivyokuwa inatua ilisindikizwa na tusi. Baadhi ya matusi ninayoyakumbuka ni, mbwa kasoro mkia, mjinga mkubwa, mpuuzi, mnyanyasaji mkubwa…. lakini katu sikumtuykania mama yake wala tusi lolote la nguoni.
Hakika nilimnyoosha sio siri!
Sauti za majirani wakinisihi nimuache nilizisikia lakini zilikuja kama kichina sikuelewa wanamaanisha nini.

“Sasa leo nakuua mbwa koko wewe!!” hili lilikuwa neno la mwisho kabisa kumweleza yule bwana kisha nikamtandika kichwa kimoja hadi mimi mwenyewe nikakumbwa na kizunguzungu!!!

Nikiwa bado katika hali ile mara ghafla nilisikia nikivutwa kwa nguvu sana nikaondolewa juu ya tumbo la yule bwana mnyanyasaji, nilipofanikiwa kugeuka kutazama ni nani aliyenitoa pale nikakutana na yule rafiki yangu askari.
“Mujuni, nini hiki rafiki yangu… we sio wa kufanya hivi kaka!!” alinisemesha huku akiniongoza kuelekea katika chumba changu.
Nilitamani kuongea lakini sikuweza, kooni bado donge la hasira lilikuwa limenikaba…
Wakati naingia ndani ndipo walau masikio yangu yaliwasikia majirani wakimzomea yule bwana kuwa kwa kipigo kile nilikuwa nimemuweza.
Tulifika ndani na yule rafiki yangu askari nikamueleza kila kitu kama kilivyokuwa, alitoka nje akamkuta Anita akiwa pale chini akiwa bado yu katika hali mbaya na hapo hakupoteza muda sheria ilichukua mkondo wake, kwanza akamtia pingu yule mwanaume. Kisha akanieleza kuwa kuwa yule Anita lazima awahishwe hospitali usiku uleule….
Ikawa kama alivyoshauri, kwa sababu Anita hakuwa na ndugu pale yule askari akanisihi niongozane naye, tukafanya vile.
Nilikumbuka kumuuliza kwanini alikuwa amewahi kumfunga pingu yule jamaa, akaniambia kuwa akibaki salama anaweza kuwahi kutoa taarifa kuwa nimempiga hivyo atanipotezea muda kuanza kuifuatilia kesi ile.
Nilikubaliana na hatua ile na kuamini kuwa ni ya msingi sana.
Tulichukua taksi hadi kituo cha polisi ambapo Anita alichukuliwa PF3 na kisha tukampeleka hospitali walipompokea.
“Mujuni eeh! Ujue leo geto kwangu shemeji yako amenitembelea sasa we kama vipi baki na huyu dada asubuhi nitafika hapa!” alinieleza askari yule na sikuwa na la kumpinga zaidi ya kucheka tu.
Nilibaki kumtazama Anita kwa ukaribu wakati akipata matibabu katika zahanati ile, uzuri ni kwamba hapakuwa na wagonjwa wengi hivyo japokuwa ilikuwa wodi ya akina mama bado niliruhusiwa kuendelea kuwemo lakini nikipewa tahadhari kuwa ikitokea akaingizwa mgonjwa mwingine nitatakiwa kutoka kwa sababu sio utaratibu.
Kufikia asubuhi Anita alikuwa mwenye nafuu kubwa alinishukuru sana kwa moyo wangu, nikamwambia kuwa asijali!! Na sikutaka kuendelea kuzungumza naye juu ya jambo hili maana natambua wazi kuwa ukaribu ukizidi yataibuka mazoea ya juu zaidi ambayo kwa lugha moja yanaitwa mapenzi. Kitu ambacho sikuwa tayari kabisa kukipokea kwa wakati ule.

*****

Baada ya majuma mawili kupita nikiwa sijajua ni kitu gani kiliendelea katika kesi ya unyanyasaji iliyokuwa inamkabili yule bwana, niliamua kumpigia simu Tito yule afande ambaye ni rafiki yangu, baada ya salamu za hapa na pale nilimuulizia juu ya maendeleo ya ile kesi akanieleza kuwa yule bwana aliachiwa huru baada ya mkewe yaani Anita kugomea mambo yale kupelekwa mahakamani na badala yake akiomba waachiwe jambo lile wakalizungumze kifamilia.
Tito alicheka sana kisha akaniambia ya wapenzi niwaachie wapenzi wenyewe…..
Nilimaliza kuzungumza naye huku nikijisemea tena kwa kurudia.
“Amakweli ya wapenzi ni kuwaachia wapenzi wenyewe”

Nikiwa bado na mshangao, niliusikia mlango wangu ukigongwa!
Nikatazama saa ilikuwa saa mbili usiku…..
Nikakumbuka kuwa nilikuwa sijalipia pesa ya umeme na maji kwa mwezi huo. Nikapatwa na mfedheheko sana, hakuna kitu nilichokuwa nachukia kama kuja kugongewa mlango na mwenye nyumba kisa kuna kitu natakiwa kulipia na sijalipia ndo maana nilikuwa nalipa mapema kabisa kodi zangu!!
Upesi nilijipekua na kutoka na shilingi elfu ishirini na tano nikaziweka mfukoni na kisha nikauendea mlango. Kweli alikuwa ni mama mwenye nyumba, nikamsalimia na kisha kumsikiliza ili akianza tu kudai chake nimpatie na kumuomba radhi kwa kuchelewesha pasipo kukusudia.
“Haujambo mwanangu Mujuni….” alinisalimia.
“Sijambo mama shkamoo….. karibu” nilimjibu….
“Mwanangu Mujuni nilikuwa nimelala si unajua tena uzee huu nawahi kulala, lakini kuna mwenzako mmoja amekujakunigongea mlango na amenieleza jambo la msingi na nikaona nikiache kitanda nije hapa kwako…” al;isita na kunitazama vyema usoni kisha akaendelea.
“Mwanangu Mjuni ukiona mtu mzima anaamua kumfata mzee kama mimi kwa ajili ya kuja kumuombea kwako ili mzungumze basi analo la msingi la kukueleza Mjuni nakuomba umsikilize mwenzako….” alimaliza kisha akageuka na kuita jina fulani ambalo sikulisikia vizuri. Na hapo nikakiona kivuli cha mwanaume kikitokea mbali kiasi. Akajongea hadi akafika tulipokuwa, na hapo nikatambua kuwa alikuwa ni Fred mume wa Anita. Alikuwa mtulivu haswa, mama mwenye nyumba akanisihi nimsikilize. Sikumpinga mama, na ningeanzaje kumpinga wakati bado nilikuwa katika mshangao…..
Nikamkaribisha ndani, akaingia taratibu akataka kuvua viatu mlangoni nikamzuia.
Akaingia na kuketi katika mojawapo ya kochi kati ya yale yaliyokuwa pale sebuleni. Alihangaika sana kuanza kuzungumza lakini alipoanza aliniomba msamaha kwa jinsia livyonivunjia heshima yangu usiku ule wa ugomvi. Nikamwambia kuwa yale yameisha….
Akatulia kwa muda kisha akaniita jina langu.
“Mujuni kaka yangu, mimi sio kijana mbaya kama ambavyo wewe na majirani wengine wanavyoweza kunifikiria Mjuni….. sipo hivyo kabisa. Hata mama yangu akifufuka leo na kuelezwa kuwa ninampiga mke wangu ama ninatukana matusi ya nguoni anaweza kufa tena tukamzika upya….. na kitakachomuua ni mshangao na mshtuko mkubwa….. hakuniacha nikiwa hivyo na aliwahi kusema wazi kuwa kati ya watu kumi wapole aliowahi kukutana nao basi na mimi ni mmouja wao. Mimi Fred ninywe pombe? Mimi niende disko? Ah wapi hicho kitu hakikuwahi kuwepo…… ila mapenzi kaka Mujuni… mapenzi kaka.” Alisita akaonekana kuzidiwa na hisia. Hakusema kitu akaufungua mlango na kutoka nje nikashindwa kumzuia, nikabaki kujiuliza tu ni kitu gani kinamkabili bwana huyu.
Nikalala nikitaraji kuwa huenda siku inayofuata atazungumza na mimi. Lakini alfajiri vilio vilisikika, na vilipozidi nikalazimika kuamka.
Fredy alikuwa amejinyonga!!!
Alijinyongea chumbani kwake huku akiacha ujumbe mfupi sana ambao hakuna aliyeweza kuuelezea maana yake, ni kama mtu aliyekuwa akiandika kwa kujilazimisha tu.
Nilichoka haswa!!!
Fredy alikuwa amekufa bila hata kunieleza ni kitu gani kilikuwa kinamsibu, mama mwenye nyumba alinihoji sana kuwa ni kitu gani marehemu alikuwa anahitaji kunishirikisha, nilimueleza mama kile kilichotokea!
Kila mmoja akabaki na jibu lake.
Ajabu, Anita hakuonekana katika tukio lile!!
Na hakuna aliyekuwa anajua nduguze Fred, hapa ndipo huwa pagumu linapokuja suala la msiba katika nyumba za kupanga.
Marafiki kadhaa wa Freddy waliokuwa wakifahamiana naye walijiunga na kukubaliana kumzika Freddy… msiba uliwekwa palepale nyumbani. Majirani tulishiriki kikamilifu katika michango ili kufanikisha kumpumzisha yule mwenzetu katika nyumba yake ya milele.
Niliendelea kuwa katika upande wa kustaajabu…. Anita hakuja msibani kabisa hadi siku ya kuzika ilipofika hakuwa ameonekana. Nilitamani kuuliza lakini ningemuuliza nani.

Wakati hili likisumbua kichwa changu, ile sikuya kuzika watu wote walioshiriki nasi waliandaliwa chakula.
Hapa nikajikuta napatwa na jambo jingine zito zaidi ambalo lilinifanya nishindwe kwenda hata makaburini pamoja na wenzangu……

*Jambo gani limetokea tena……
Usikose kuungana nasi katika muendelezo wa simulizi hii.

No comments:
Write comments

Recommended Posts × +