Matatizo ya kukosa au kupungua hamu ya kujamiana yanatambulika kama tatizo linalojirudia kwa muda mrefu ambapo huathiri mzunguko wa tendo la kujamiana (kusisimka, kufikia kilele, kurudia) na hivyo kusababisha msongo wa mawazo au kuharibu uhusiano kati ya mtu na mwenza wake. Katika makala hii, mwandishi wako Dk. Khamis Hassan anachambua vitu vinavyoweza kusababisha tatizo hili na jinsi ya kuliepuka.
Kupungua au kukosa hamu ya kufanya mapenzi ni suala linaloonekana kuathiri wenza wengi. Jamii imeshuhudia visa vingi vinavyosababishwa na mwenza mmoja kutoka nje ya ndoa au uhusiano kwa kisingizio cha kutoridhishwa na utendaji wa mwenzake katika suala la kujamiana. Kadhalika jambo hili limesababisha kuvurugika kwa ndoa nyingi na wakati mwingine kusababisha magonjwa au hata vifo kwa mmoja au wenza wote wawili.
Lakini nini hasa sababu ya kuwepo kwake?
Kwa ujumla visababishi vya tatizo hili kwa wanaume na wanawake ni pamoja na msongo wa mawazo uliokithiri. Asilimia kubwa ya ukosefu wa hamu ya kujamiana husababishwa na msongo wa mawazo unaompata mwenza mmojawapo kwa sababu ya ugumu wa maisha (uchumi), matatizo katika uhusiano (ugomvi, kutoelewana, kutoaminiana au kukosa uaminifu katika uhusiano {infidelity} n.k) au magonjwa mbalimbali. Sababu nyingine ni kupungua au kukosekana upendo/mapenzi katika uhusiano/ndoa, unywaji pombe kupindukia, na utumiaji wa dawa za kulevya.
Aidha kujifungua mtoto nako kunaelezwa kuwa ni chanzo kingine cha kuwepo kwa tatizo hili kwa wanawake. Hii inatokana na ukweli kuwa, mama anaponyonyesha, homoni aina ya prolactin huwa katika kiwango cha juu. Pamoja na kazi nyingine za Prolactin, homoni hii pia humfanya mtu kuridhika baada ya kujamiana (sexual refractory period) kwa kuingiliana na ufanyaji kazi wa homoni nyingine ya dopamine ambayo humfanya mtu kufikia kilele.
Sababu nyingine ni kupungua kwa mzunguko wa damu katika sehemu za siri za mwanamke na hivyo kumsababishia maumivu wakati wa kujamiana, na kwa wanawake wenye matatizo ya homoni ya tezi la thyroid yajulikanayo kama hypothyroidism hupatwa na tatizo hili zaidi kuliko wanaume. Wapo baadhi ya wanawake wanaokumbwa na tatizo la vaginismus ambalo husababisha sehemu za siri za mwanamke kuwa ndogo wakati wa kujamiana na hivyo kumsababishia maumivu makali na kumfanya akose hamu ya kujamiana tena.
Aidha utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi au vya majira kwa muda mrefu (kwa wanawake), ugonjwa wa kisukari (wa wanaume na wanawake), uzito uliopitiliza (obesity) pamoja ugonjwa wa viungo vya mifupa yaani arthritis navyo vinaelezwa kuwa chanzo cha kuwepo kwa tatizo hili.
Ujauzito pia unaelezwa kuwa sababu nyingine ya baadhi ya wanawake kukosa hamu ya kujamiana. Hii inatokana na kuwepo kwa mabadiliko katika mfumo wa homoni na maumbile ya wanawake wakati wa ujauzito, hali inayowafanya baadhi ya wanawake kutojiamini.
Wanawake waliowahi kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi (hysterectomy) na kusababisha madhara katika neva inayohusika na kuongeza msisimko wakati wa kujamiana (pudendal nerve damage) huwa katika hatari ya kupata tatizo hili. Madhara ya neva hii pia huonekana hata kwa wanaume.
Visababishi vingine ni pamoja na madhara yatokanayo na matumizi ya baadhi ya dawa kama vile za kutibu shinikizo la damu (antihypertensives), msongo wa mawazo (antidepressants) na saratani; kuwa na ugonjwa wa moyo, saratani ya aina yoyote ile, au kuwa na wasiwasi (anxiety).
Kwa wanawake, uchovu unaotokana na kuzidiwa na majukumu ya kulea mtoto/watoto, kazi na kumhudumia mume wake nao unaweza kuchangia kukosa hamu ya kujamiana. Aidha mwanamke mwenye historia ya kubakwa, au aliyewahi kupata maumivu wakati wa kujamiana siku za awali kutokana na kutokuwa tayari kujamiana au kutotayarishwa vyema naye pia ana hatari ya kukumbwa na tatizo hili.
Kupenda mtandao (internet) kupita kiasi (internet addiction) nako kumeelezwa kuwa sababu nyingine ya kuwafanya wenza kukosa hamu ya kujamiana. Kwa mujibu wa utafiti mmoja uliofanyika mwaka 2011 huko nchini Marekani, ilionekana kwamba kati ya ndoa 6,000 zilizovunjika, asilimia 57 ya ndoa hizo zilisababishwa na mwenza mmoja au wote wawili kupenda kuchat au kutumia mtandao kupita kiasi na hivyo kusababisha kupotea kwa msisimko kati ya wenza na hatimaye kupungua uwezo au hamu ya kujamiana.
Uvutaji sigara ni chanzo kingine cha kukosa au kupungua hamu ya kujamiana na huathiri wote wanaume pamoja na wanawake. Uvutaji sigara hupunguza vichocheo aina ya testerone kwa wanaume, na kitendo cha kuwa na kiwango kidogo cha homoni hii husababisha wavutaji sigara wengi kupata tatizo la kupungukiwa uwezo wa kujamiana. Kadhalika uvutaji sigara hupunguza mzunguko wa damu unaopita kwenye uume hivyo kumfanya muhusika kushindwa kusimika au jongoo kushindwa kupanda mtungi (vascular impotence) na hatimaye kukosa uwezo wa kujamiana. Kwa wanaume, uvutaji sigara hupunguza kiwango na uzito wa shahawa (concentration of spermatozoa in semen) kwa takribani asilimia 22-57, wakati uwezo wa mbegu za kiume kuogelea kufikia mirija ya uzazi ya mwanamke nao pia hupungua kwa asilimia 20 ikilinganishwa na wasiovuta. Aidha tafiti kadhaa zimethibitisha uvutaji sigara unaweza kusababisha kuzalishwa kwa mbegu za kiume zisizo na maumbile ya kawaida hivyo kuongeza uwezekano wa kuharibika kwa mimba itakayotungwa (spontaneous abortion) au kuzaliwa kwa mtoto mwenye hitilafu za kimaumbile (birth defects). Pia uvutaji sigara uharibu mirija ya seminiferous tubules (sehemu ambapo mbegu za kiume hutengenezwa) iliyopo kwenye korodani na hivyo hupunguza wingi na uzito wa mbegu hizo. Mambo haya huweza kumfanya mwanaume ajihisi aibu kufanya mapenzi na mwenza wake hali ambayo ikiendelea kwa muda mrefu huwa sugu na kusabsbisha kukosa hamu ya kujamiana moja kwa moja.
Sababu nyingine ni pamoja na umri kuwa mkubwa. Wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 40 huwa na ongezeko kubwa la kiwango cha homoni ya prolactin ambayo husababisha kuongezeka kwa kichocheo kingine cha dihydro-testerone inayosababisha kuvimba kwa tezi dume hatimaye kupunguza uwezo wa kusimika kwa mwanaume, na mwishowe kukosa au kupungua hamu ya kujamiana.
Na mwisho ni tabia ya kuendesha baiskeli kwa muda mrefu (kwa kipindi kimoja) ambayo hugandamiza neva na mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye uume na kusababisha mtu kupungukiwa na uwezo wa kusimamisha kwa muda na hatimaye kupungukiwa hamu ya kujamiana.
Vipimo vya uchunguzi
Ili kuweza kutambua chanzo cha tatizo hili, daktari huchukua historia ya maisha ya mhusika kwa ujumla, historia yake inayohusisha matumizi ya dawa aina mbalimbali, historia yake ya maisha ya ngono (sexual history) pamoja na kuchunguza dalili za magonjwa mbalimbali. Historia ya mgonjwa husaidia sana katika kufahamu ni vipimo na uchunguzi gani ufanyike. Vipimo hivyo vinaweza kuwa
Vaginal swab kwa ajili ya kuchunguza magonjwa ya zinaa au magonjwa mengine sehemu za siri za mwanamke
Uchunguzi wa mkojo (urinalysis)
Uchunguzi wa uwepo wa mabadiliko sehemu za siri za mwanamke kama vile mabadiliko ya kimaumbile (physical changes) kusinyaa kwa njia (thinning of genital tissues) kuwepo kwa makovu (scarring) na kupungua kwa hali ya kuvutika na ulaini wa ngozi ya sehemu hizo (decreased skin elasticity)
Kumpima akili mhusika
Kuchunguza kiwango cha homoni mbalimbali kama vile T3, T4 (kutoka tezi ya thyroid), testosterone (kutoka kwenye korodani), homoni ya ukuaji na homoni ya prolactin.
Uchunguzi wa shahawa (semen analysis) ambayo hujumuisha kuchunguza wingi wake (volume), kiwango chake (sperm count), mvutano wake (liquefaction time), maumbile ya mbegu (sperm morphology), pH yake, uwezo wa mbegu kuogelea (sperm motility), kiwango cha sukari na chembechembe nyeupe za damu.
Uchunguzi iwapo mhusika ana uzito unaolingana na urefu wake (body mass index, BMI) kulingana na umri wake
Vipimo vya ugonjwa wa shinikizo la damu hususani kwa wale wenye ugonjwa huo au wenye dalili zake au wale wanaotumia dawa za shinikizo la damu
Vipimo vya ugonjwa wa kisukari kama vile fasting blood glucose test (FBG), Oral Glucose Tolerance Test (OGTT), na glycosylated hemoglobin (Hb A1C).
Je, tatizo hili linatibika?
Ndiyo! Habari njema ni kwamba tatizo la kupungua au kukosa hamu ya kufanya mapenzi linatibika kabisa. Jambo la muhimu ni kufahamu chanzo chake na kukishughulikia. Tiba inaweza kuhusisha mambo kama
Kubadilisha mfumo wa maisha
Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kuongeza stamina, hupunguza uzito, kumfanya mtu kuwa na umbile zuri, furaha na kuongeza ufanisi wakati wa kujamiana
Kupunguza msongo wa mawazo kwa kukubali kwamba lipo tatizo baina ya wenza na hivyo kutafuta suluhu pamoja na kuacha ugomvi. Fahamu kwamba malumbano na matatizo ni vitu vya kawaida katika uhusiano wowote. Ni vizuri kwa wenza kukaa pamoja na kuzungumza matatizo yao, kuwa wakweli, waaminifu na kuaminiana, kujaliana na kuzungumza juu ya tendo la ndoa kwa pamoja. Ni vizuri kila mmoja kuainisha vitu anavyopenda na asivyopenda kufanyiwa wakati wa kujamiana. Pale inapotokea mmoja hajapendezwa au kufurahishiwa na uwajibikaji au ufanisi wa mwenzake hana budi kutumia lugha nzuri kutafuta kiini cha tatizo na kulitafutia ufumbuzi.
Pia matatizo ya kimaisha (fedha, nk) hayana budi kuzungumzwa kwa pamoja baina ya wenza na kisha kutafutiwa ufumbuzi
Kufanya mazoezi ya misuli ya nyonga (pelvic muscles) kwa kufanya kama unazuia mkojo wakati unahisi haja ndogo na kuhesabu moja hadi tano, baada ya tano pumzika na halafu rudia tena. Mazoezi ya namna hii (Kegel’s exercise) huongeza uwezo wa kujamiana kwa wanawake.
Weka mazingira mazuri na muda wa kufanya tendo la ndoa na mwenza wako ili mpate kudumisha uhusiano wenu
Ongeza msisimko katika uhusiano wenu kwa kujaribu aina, mbinu na mikao mbalimbali wakati wa kujamiana, kubadili muda wa kufanya mapenzi (siyo lazima usiku tu mnaweza fanya hata asubuhi au mchana) au sehemu tofauti na ile mliyozoea (si kila siku kitandani)
Kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa mambo ya uhusiano na ndoa (marriage counsellors) na hata madaktari wa magonjwa ya akili kwani wao ni weledi zaidi katika masuala haya
Tiba kwa kutumia dawa
Iwapo ugonjwa ambao ni kiini cha tatizo hili unafahamika kwa mfano kisukari, magonjwa ya moyo, au magonjwa ya zinaa, unafahamika, ni vema utibiwe ipasavyo
Daktari kumbadilishia mhusika dawa zinazoleta madhara kama ya msongo wa mawazo, shinikizo la damu au za saratani n.k.
Kutibu tatizo la msongo wa mawazo (depression) na hali ya kuwa na hofu na mhemko (anxiety)
Kwa wanawake wanaopata maumivu wakati wa kujamiana au wenye sehemu za siri zilizo kavu (dryness of vagina) au zenye kuwasha (irritation), wanashauriwa kutumia dawa au jelly (vaginal lubricants) zinazolainisha maeneo hayo wakati wa tendo hilo
Tiba ya homoni yaani Estrogen Replacement Therapy (ERT) au androgen therapy kwa wale wenye tatizo hilo
Na matumizi ya dawa ya Yohimbine Hydrochloride
Je, ni kweli kuwa kuna vyakula vinavyosaidia kupunguza tatizo hili?
Bila shaka, vipo! Ifahamike kuwa vyakula hivi siyo tiba mbadala bali hunasaidia kuongeza ufanisi na ubora kwa wale wenye tatizo la kupungua au kukosa hamu ya kujamiana. Aidha huwafaa hata wale wasio na tatizo hili bali wanataka tu kudumisha uhusiano na wenzi wao. Vyakula hivyo ni pamoja na;
Kitunguu swaumu yenye kemikali ya allicin kwa wingi inayoongeza hamu ya kujamiana na uzalishaji shahawa.
Figili ambayo huchochea hamu ya kujamiana kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha homoni ya androsterone.
Habat al soda (black caraway seeds)
Ndizi ambayo ina kimeng’enyo cha bromelain kwa wingi na madini ya potassium ambayo huongeza msisimko wa kujamiana kwa wanaume.
Mayai na chocolate
Vyakula vyote vyenye vitamin A, B complex, C, na E kama vile nyanya/tungule, pamoja na vyakula vyenye madini ya Zinc, selenium, magnesium, calcium kama vile karanga
Mdalasini (Cinammon stick) pamoja na Asali.
Thursday, April 25, 2019
KUPUNGUA AU KUKOSA HAMU YA KUFANYA MAPENZI (LOW OR LOSS OF SEXUAL LIBIDO)
Posted by
NeverGoBack
on
4:39 AM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Write comments